MKAKATI wa Edward Lowassa kutaka kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huenda ukakwama baada ya baadhi ya vigogo ndani ya chama hicho kupanga mkakati wa kutaka kumfukuza, imefahamika.
Taarifa za ndani ya CCM zinasema mpango wa kutaka kumfukuza Lowassa kutoka chama chake unatokana na hofu ya baadhi ya wagombea wenzake wanaohaha kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015.
Vyanzo vya habari zetu vimemnukuu mmoja wa vigogo waandamizi ndani ya chama hicho akisema, mkakati wa kumvua Lowassa uanachama unasukwa kwa ustadi mkubwa na kigogo mmoja mwandamizi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na serikali.
“Huyu bwana tayari ameanza mikutano ya kampeni, hata kabla ya chama chetu kutoa mwongozo. Anazunguka nchi mzima kusaka urais. Huku ni kuvunja taratibu. Tutakutana na kumdhibiti,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili kwa sharti la kutotajwa gazetini.
Taarifa zinasema mkakati wa kumfukuza Lowassa utaegemea hoja kuu mbili:
Kwanza, ni madai kuwa Lowassa ameanza kampeni kabla ya chama chake kutoa mwogozo; kujenga mtandao wa ushindi na kudaiwa kupanga safu za uongozi; jambo ambalo linaweza kukidhoofisha chama chake.
Kuhusu tuhuma za kuanza kampeni mapema, mtoa taarifa anasema, Lowassa anatuhumiwa, pamoja na mambo mengine, kuzunguka nchi nzima kufanya mikutano na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wenyeviti wa mikoa na makada wengine wa ngazi za kati na kuwashawishi kumuunga mkono katika mbio zake za kusaka urais.
Hata hivyo, mkakati wa kumfukuza Lowassa kwa madai ya kuanza kampeni mapema waweza kukwama kwa kuwa mmoja wa wagombea anayepigiwa chapuo na walioko madarakani, naye tayari ameanza kampeni.
Pili, mkakati wa kumfukuza Lowassa, unatajwa kujikita kwenye madai ya kuhusika kwenye ufisadi wa mkataba tata wa kufua umeme wa kampuni ya Richmond Development Company (RDC).
Wakati mkabata huo unafungwa, Lowassa alikuwa waziri mkuu wa Jamhuri. Alitajwa na Kamati Teule ya Bunge, kwamba ndiye aliyeshinikiza watendaji serikalini kuipa kampuni hiyo kazi ya kufua umeme. Ilithibitika baadaye kuwa kampuni haikuwa na uwezo, ujuzi wala sifa ya kufanya kazi iliyopewa.
Mtoa taarifa anasema, ni mara baada ya mkutano ambapo taarifa zake zilivuja kwenye chama na serikalini na mpango wa kumfukuza ukafufuliwa upya.
mwandishi wetu alipowasiliana na kiongozi mmoja mstaafu serikalini kuhusu kufukuzwa kwa Lowassa na iwapo mkakati huo unaweza kufanikiwa, haraka alisema, “Hata mimi nimesikia. Nami nimewauliza kama ambavyo unaniuliza wewe, kwamba ‘mtaweza?’”
Anasema amewaambia kuwa huyu bwana (Lowassa) tayari amejijenga ndani ya chama na kwamba hatua yoyote ya kumfukuza sasa inaweza kukivuruga zaidi chama hicho.
Akiongea kwa hasira kigogo huyo alisema, “Huyu bwana (Edward Lowassa), anataka kutuharibia chama chetu. Lazima tumfukuze. Tutaitisha vikao vya Kamati Kuu (CC) na NEC kumjadili. Tunataka tulifanye hili kabla ya mambo kuharibika zaidi.”
Hata hivyo, wapinzani wa mkakati wa kumfukuza Lowassa wanasema, kufanikiwa kwa mpango huo kutakigharimu mno CCM kuliko kumuacha Lowassa hadi mwisho akapigiwa kura na kukataliwa na wajumbe wa vikao vya vyama, mtoa taarifa anasema, Lowassa alitangazia wafuasi wake kuwa ameanza mbio za kutafuta urais; aliahidi kupambana hadi mwisho.
Kuibuka kwa taarifa hizi za kutaka kumdhibiti Lowassa kwa tuhuma za kuanza kampeni kabla ya muda, kumekuja wiki tatu baada ya gazeti hili kuanika orodha ya watu 14 wanaotajwa kutaka kuwania urais, miongoni mwao wakiwa wale wanaodaiwa kuwa tayari wameanza kampeni.
Miongoni mwa wanaotajwa kuanza kampeni, ni Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emanuel Nchimbi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Steven Wassira na aliyepata kuwa waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Katika mbio hizo, Membe anatajwa kuunganisha nguvu na Migiro kwa upande mmoja na Samwel Sitta kwa upande mwingine.
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, muungano kati ya Membe na Sitta unasukumwa na agenda ya kukabiliana na nguvu ya Lowassa.
“Hata muungano kati ya Membe na Migiro, nao ni kama muungano kati ya Membe na Sitta. Yote hii, inasukumwa na kukabiliana na Lowassa. Sasa ikitokea Lowassa akakatwa mapema, nao hawa wataanza kukimbiana, kila mmoja akitafuta urais kivyake. Maana wataona yule anayewanyima usingizi tayari atakuwa ameshaondoka,” ameeleza mtoa taarifa wetu.
Anasema, “Hata hawa, kama alivyo Lowassa, tayari wameanza kampeni. Mwishoni mwa mwezi uliopita, Membe alikuwa Iringa, ambako pamoja na mambo mengine alikutana na makundi mbalimbali ya watu na kutangaza kugombea urais,” ameeleza kigogo mmoja wa chama hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini
No comments:
Post a Comment